Mzee Kulwa ni mkulima maarufu sana katika kijiji cha
Gagagege. Yeye na familia yake pia ni wafugaji. Kijiji cha Mzee Kulwa kiko kandokando mwa ziwa, hivyo mzee huyu pamoja na jirani zake wanavua samaki pia, hasa wakati wa masika.
Mzee Kulwa hivi sasa ana umri wa kama miaka tisini.
Tunakisia umri wake kwani
anakumbuka kwamba alipokuwa mwenye umri wa "kuchunga ng'ombe", Waingereza walianza kutawala Tanzania. Ingawaje uzee umepunguza nguvu za Bwana Kulwa, bado anaweza kufanya kazi shambani na hupenda sana kwenda ziwani na wajukuu zake na huwafundisha
Kigagagege.
Wagagagege ni watu wataratibu sana na bado wanafuata mila zao za zamani. Mzee Kulwa ni kiongozi wa shirika la wazee. Wazee wa kijiji hiki
wanaheshimiwa sana na wanakijiji. Wazee hawa bado wana sauti kubwa katika mipango ya maendeleo ya kijiji, na wanajadili na kuhukumu kesi ndogondogo za wanakijiji. Ingawaje Mzee Kulwa amekubali mabadiliko na maendeleo ya kijiji chake, bado anasisitiza sana vijana watunze na kuheshimu mila na desturi za kabila lake. Hata leo, Mzee Kulwa hasiti kumsema na hata kumuadhibu yeyote kijijini!
Tumtakie Mzee Kulwa na Wazee wengine kama yeye maisha mema na yenye furaha.